Catholic Diocese Malindi

slider10.jpg
slider5.jpg
slider8.jpg
slider6.jpg
slider11.jpg
slider9.jpeg
previous arrow
next arrow

Baraza la Kidini la Kenya (IRCK) lina wasiwasi mkubwa kuhusu utekaji nyara wa watu saba waombaji hifadhi kutoka Uturuki mnamo tarehe 18 Oktoba 2024 jijini Nairobi. Watu hao—Mustafa Genç, mwanawe Abdullah Genç, Hüseyin Yeşilsu, Necdet Seyitoğlu, Öztürk Uzun, Alparslan Taşçı, na mkewe Saadet Taşçı waliripotiwa kutekwa nyara na watu wasiojulikana.

Ingawa Abdullah Genç, Necdet Seyitoğlu, na Saadet Taşçı wameripotiwa kuachiliwa, Öztürk Uzun, Alparslan Taşçı, Mustafa Genç, na Hüseyin Yeşilsu bado hawajulikani waliko na wako katika hatari kubwa ya kurejeshwa kwa lazima

 Jambo ambalo ni ukiukaji mkubwa wa sheria za kimataifa. Baadhi ya watu hawa wameishi kwa amani nchini Kenya na wanajulikana kwetu, pamoja na Wakenya wengi, kama watu wenye kupenda amani ambao wamejihusisha na kazi za misaada na shughuli za kibinadamu kwa miaka mingi ili kusaidia makundi yenye uhitaji nchini Kenya.

Tukio hili linakiuka sheria za wakimbizi za Kenya na za kimataifa. Watu hawa ni wakimbizi waliotafuta ulinzi wa serikali ya Kenya. Utekaji nyara wao unasababisha wasiwasi kuoongezeka kuhusu usalama wa wakimbizi wote na waombaji hifadhi nchini Kenya.

Serikali ya Kenya inapaswa kuchukua hatua za haraka kuwatafuta waombaji hifadhi wa Kituruki waliopotea, kuhakikisha usalama wao, na kuzuia kurudishwa kwa nguvu nchini Uturuki ambako wako katika hatari kubwa ya kuteswa.

IRCK linaungana na mashirika ya haki za binadamu ya ndani na ya kimataifa ambayo yamezungumza na kutoa taarifa kuhusu tukio hili la kusikitisha kuomba Umoja wa Mataifa na jamii ya kimataifa kulifuatilia tukio hili. Inatisha kwamba haya yanatokea katika mwezi ambao Kenya imefanikiwa kuomba kuwa mwanachama wa Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa.

Tukio hili linaashiria mwenendo unaotia wasiwasi nchini Kenya. Nchi ambayo hapo awali ilihesabiwa kuwa kimbilio salama kwa wakimbizi sasa inageuka kuwa mazingira hatari na yenye uhasama kwa wale wanaotafuta hifadhi.

Tunaiomba Serikali ya Kenya kuhakikisha kwamba waombaji hifadhi na wakimbizi wote wanalindwa dhidi ya utekaji nyara wa kihalifu na kurejeshwa kinyume cha sheria katika nchi ambako maisha yao na uhuru wao viko hatarini. Serikali inapaswa kutekeleza majukumu yake ya kisheria chini ya Katiba ya Kenya, sheria za wakimbizi, na mikataba ya kimataifa ya haki za binadamu.

IMESAINIWA NAWAAKILISI WA IRCK, MALINDI/KENYA