Catholic Diocese Malindi

slider10.jpg
slider5.jpg
slider8.jpg
slider6.jpg
slider11.jpg
slider9.jpeg
previous arrow
next arrow

WAT. LEONARDI NA WENZAKE,

WAFIADINI WA GORIKUM
( 7 JULAI )

Zamani zile watu wa Uholanzi walipomwasi mfalme wao Filipo wa Hispania, Waprotestanti walitaka dini Katoliki ikomeshwe nchini mwao. Walikuwa wakiingia ndani ya Makanisa, wakivunja sanamu na kutenda kufuru nyingi. Mjini Gorikum walikaa mapadre kumi na tisa, Leonardi na wenzake. Wahalifu wale waliuteka mji wa Gorikum wakawakamata Mapadre wote na kuwafunga bomani. Usk ulipoingia, wafitini hao, baada ya kulewa sana waliwatoa Mapadre hao wakawavua mavazi yao, wakawatesa vikali ili waikane dini yao. Waliwashurutisha kwa nguvu kusudi Mapadre waseme kuwa Bwana wetu Yesu Kristo hayumo katika Sakramenti ya Ekaristi; wamkane Baba Mtakatifu na kadhalika. Lakini Mapadre na Wamonaki walikaa imara. Ndipo makafiri wakawafunga Mapadre kamba shingoni na

kuwatundika ukutani mwa mlango, wakiwasukuma huku na huko na kupiga kelele. Mwili wa Padre Mkuu wa Wakapuchini ukaanguka chini; hapo askari walitwaa mwenge wa moto wakachoma kichwa, masikio, pua na midomo ya shahidi Mtakatifu. Wakidhani kuwa amekufa, wakaenda zao. Lakini Padre huyu hakufa, pole pole fahamu zilimrudia tena.

Baada ya siku kumi Mashahidi Watakatifu walipakiwa merikebuni wakasafirishwa mpaka bandari ya Brielle. Huko, Lumey, kapteni wa wanyang'anyi, aliyekuwa adui mkubwa wa Wakatoliki, aliwangonjea. Walipofika walipelekwa sokoni, na njiani walipigwa na wahalifu; wafitini wa dini waliwatukana, wakiwa kuwatupia mawe. Lumey mwenyewe aliwapiga mijeledi ya usoni. Wakati huo mashahidi waliimba Litania ya Watakatifu.

Hatimaye, walikokotwa nje ya mji. Ndipo waliponyongwa kwa kamba, wakafa. Watesi waliikata miili yao vipande vipande. Ilikuwa tarehe 9 Julai, mwaka 1572. Majina ya wafiadini ni: Leonardi, Andrea, Yakobo, Adriano, Yeronimo, Teodori, Nikasi, Wilehad, Fransisko, Petro, Korneli, Nikola (wawili wenye jina hilo), Godefridi (wawili), Yohani (wawili), na Antoni (wawili). Papa aliwaandika katika orodha ya Watakatifu mwaka 1867.

WAT. LEONARDI NA WENZAKO, MTUOMBEE.

MASOMO YA MISA

I. Mwa 23:1-4,19; 24:1-8,62-67

Zab. 106:1-5

INJILI. Mt. 9:9-13