slider10.jpg
slider5.jpg
slider8.jpg
slider6.jpg
slider11.jpg
slider9.jpeg
previous arrow
next arrow
New CWA members of Marafa Deanery

Leo, katika parokia ya Magarini Mhashamu Askofu Willybard Lagho aliongoza Misa Takatifu katika deanery ya Marafa. Huku akiwahimiza waumini, hasa wazazi, kuhusu umuhimu wa kushirikiana katika malezi ya watoto wao. Askofu Lagho alisisitiza kuwa malezi sio jukumu la mzazi mmoja tu bali ni jukumu la wazazi wote wawili, na kwa ushirikiano wao, wanaweza kuwalea watoto katika njia inayofaa.

Askofu Lagho aliwasihi wazazi kuwa mfano bora kwa watoto wao. Alisema, "Wazazi, watoto wenu wanawaangalia na kujifunza kutoka kwenu. Jitahidini kuwa mfano mzuri kwao. Watoto wenu wanahitaji kuona maadili mema na tabia njema ndani yenu ili waweze kuyafuata." Aliendelea kusisitiza kwamba watoto wanahitaji kulelewa katika imani ya Kikristo, wakijua na kufuata mafundisho ya Yesu Kristo. "Imani inapaswa kuwa msingi wa maisha yao," aliongeza. "Ni muhimu sana kuwafundisha watoto wetu kumjua na kumpenda Mungu tangu wakiwa wadogo."

Katika hotuba yake, Askofu Lagho pia alihimiza heshima kwa watu wote. Alisema, "Tufundishe watoto wetu kuwaheshimu watu wote, bila kujali tofauti zao. Heshima ni msingi wa upendo na umoja katika jamii yetu."

Misa hiyo pia ilishuhudia wanaume 13 wakipokelewa katika kundi la Catholic Men Association na kina mama wakipokelewa katika kundi la Catholic Women Association. Askofu Lagho aliwapongeza wanachama wapya na kuwasihi waige mfano wa wenzao katika majimbo mengine, hasa katika masuala ya michango ya kufadhili miradi ya jimbo. Alisema, "Tunahitaji kuwa na umoja na kushirikiana katika kufanikisha miradi yetu ya kijimbo. Michango yenu ni muhimu sana katika kufanikisha malengo yetu."

Baba Askofu pia aliwataka waumini watafute mbinu mbadala za kufanya michango. "Tafuteni njia mpya na bunifu za kuchangia, ili tuweze kutekeleza miradi yetu kwa ufanisi zaidi," alihitimisha.

Misa hiyo ilimalizika kwa furaha na shangwe, huku waumini wakiwa na moyo mpya wa kushirikiana na kujitolea katika maendeleo ya parokia na jimbo lao.