Utekaji nyara wa raia saba wa uturuki, umezua maswali mengi na hofu miongoni mwa wananchi na viongozi mbalimbali humu nchini na ulimwenguni. Utekaji nyara huo ulifanyika hivi majuzi jijini Nairobi na kufikia sasa raia hao wa Uturuki hawajulikani waliko.
Viongozi wa kidini mjini Malindi kaunti ya Kilifi wamekemea vikali utekaji nyara wa raia hao wa Uturuki, wakisema unahujumu usalama wa taifa la Kenya.
Viongozi hao wa kidini, wakiongozwa na Baba Askofu Willybard Lagho, Askofu wa jimbo letu la Malindi, wamegadhabishwa na kisa hicho wakisema mambo kama hayo yanazua hofu miongoni mwa wananchi na pia watalii wanaozuru taifa la Kenya.
“Kenya inatumbukia mahali pasipo pazuri ambapo raia wake hawana usalama. Kama tulivyokemea utekaji nyara wa Genz wakati wa maandamano, tunazidi kuiomba serikali na viongozi wetu kutia jitihada ili kukomesha mtindo wa watu kutekwa nyara. Ni mtindo ambao unaleta hofu nyingi na unaweza kuharibu sifa ya nchi ambayo inategemea utalii kama nguzo moja ya kiuchumi’’, alisema Askofu Lagho.
Vile vile Sheikh Famau Mohammed Famau, ambaye ni kiongozi wa dini ya kiIslamu mjini Malindi, amesema jambo hili linafaa kuchukuliwa hatua maana linahatarisha usalama wa nchini. “Ni jambo ambalo linahatarisha uhusiano wa kimataifa. Nchi ya Kenya iko na sheria zake na mtu yeyote ambaye amepatikana na hatia, ni vyema apelekwe mahakamani, na akipatikana na makosa basi sheria ichukuwe mkondo wake badala ya watu kutekwa nyara. Inasikitisha kuona kwamba leo sheria za nchi zinavunjwa” alisema Sheikh Famau.
Vilevile Askofu wa kanisa la kiAnglikana jimbo la Malindi, Askofu Reuben Katite, ameiomba serikali kuliangazia swala hilo kwa kina, “Serikali iwe makini sana na jambo hili la utekaji nyara kwa raia na hata wale ambao si raia wa Kenya, kwasababu mahali ambapo kuna mambo ya utekaji nyara, ni vigumu kwa watalii kuja kutalii na kutuletea fedha ambazo tunazihitaji sana katika taifa letu. Tunazidi kuiomba serikali kutilia maanani swala hili na kuhakikisha kwamba, visa hivi vya utekaji nyara vimeondolewa kabisa”, alisema Askofu Reuben.