Catholic Diocese Malindi

slider10.jpg
slider5.jpg
slider8.jpg
slider6.jpg
slider11.jpg
slider9.jpeg
previous arrow
next arrow

*MAISHA YA WATAKATIFU*

*MT. BONAVENTURA,*
ASKOFU NA MWALIMU WA KANISA
( 15 JULAI )

Mtakatifu Bonaventura alizaliwa mwaka 1218 katika Mkoa wa Toskana (Italia). Siku ya ubatizo wake aliitwa Yohane. Alipopata umri wa miaka minne aliugua ugonjwa mkali, akawa karibu kufa. Ndipo mama yake akamwangukia Mtakatifu Fransisko wa Asizi amwombee mwanae kwa Mungu, akaweka nadhiri kumtolea kwa Mungu katika Shirika la Wafransisko ikiwa atajaliwa kupona. Mtakatifu Fransisko alisali, na mtoto akapona. Baadaye, siku moja Fransisko alipita huko Toskana, akaja akamtazama mtoto yule aliyepona kwa sala zake. Alimpokea mikononi mwake akisema kwa furaha: "Ee, Bouna Ventura", ndio kusema: "Ee, Bahati njema". Na toka siku ile mtoto aliitwa Bonaventura.

Alipopata umri wa miaka ishirini na mmoja aliingia katika Shirika la Ndugu Wafransisko kama alivyokuwa ameahidi mama yake. Alipelekwa kusoma Falsafa na Teolojia katika Chuo Kikuu cha Paris (Ufaransa), na mwisho akawa mwalimu pale pale. Mtakatifu Toma wa Akwino alikuja kumtazama siku moja akamwuliza: "Uniambie, Bonaventura, katika vitabu gani umejifunza yote haya? " Bonaventura alimjibu akimwonyesha msalaba uliokuwa mezani kwake: "Msalaba huu ndiyo kitabu changu bora. Nimejifunza zaidi kwa kusali mbele ya Msalaba kuliko kwa kusoma vitabu".

Kisha alichaguliwa kusimamia Shirika lote wa Wafransisko. Akalisimamia kwa hekima na busara kubwa. Naye Papa alimfanya kuwa Askofu na Kardinali wa Albano (Italia). Ingawa hivyo, hakuwa mtu mwenye makuu kama inavyosimuliwa katika hadithi ifuatayo: Alipoteuliwa kuwa Kardinali, wajumbe walitumwa na Papa kumpelekea kofia ya Kikardinali. Walipotaka kumpa, akawaambia wakaitundike mtini hapo karibu, kwa maana alisema ana shughuli ya kuosha sahani, kwa hiyo mikono yake imeloa na ina mafuta.

Mtakatifu Bonaventura aliandika vitabu vingi maarufu vya Falsafa na Teolojia. Alijishughulisha sana kupatanisha Kanisa la Kigiriki na la Kiroma katika Mtaguso wa Lioni (Lyon, Ufaransa). Kazi hizi zote zilimwelemea sana, akafa wakati wa Mtaguso mwaka 1274, akazikwa huko Lioni. Alitangazwa kuwa Mtakatifu mwaka 1482, na Mwalimu wa Kanisa mwaka 1588.

*MT. BONAVENTURA, UTUOMBEE*

*MASOMO YA MISA*

I. Mwa 49:29-33; 50:15-25

Zab. 105:1-4,6-7

INJILI. Mt. 10:24-33