Catholic Diocese Malindi

slider10.jpg
slider5.jpg
slider8.jpg
slider6.jpg
slider11.jpg
slider9.jpeg
previous arrow
next arrow

*MAISHA YA WATAKATIFU*

*MT. SIRILI WA ALEKSANDRIA,*
ASKOFU NA MWALIMU WA KANISA
( 27 JUNI )

Sirili alizaliwa mwaka 370. Aliingia utawani na baadaye akapewa Upadre. Mjomba wake alikuwa Teofili, Askofu wa Aleksandria (Mji mkuu wa Misri), ambaye wakati ule alishika nafasi ya kwanza katika Makanisa ya Mashariki. Sirili alimfuata mjomba wake kama Askofu wa Aleksandria, na aliliongoza jimbo lake kwa ujasiri ambapo kulitokea usumbufu mkubwa. Mambo hayo yote yalisababisha mwanzo mgumu kwa mtu aliyetaka kutoa utumishi katika Kanisa kutokana na elimu na bidii yake ya kuwaunganisha Wakristo.

Katika mwaka 438, Nestori, Padre mtawa, aliteuliwa kuwa Askofu Mkuu wa Konstantinopoli (Uturuki). Askofu huyu alifilundisha kuwa kuna nafsi tofauti katika Kristo, ile ya Mungu na ile ya mtu. Kadiri ya mafundisho yake, Mungu alikaa ndani ya Yesu kama alivyokaa Kanisani. Kwa hiyo, alisema kwamba Mungu hakujifanya mtu kwa njia ya Mwanae. Alifundisha pia kwamba Bikira Maria hakuwa Mama wa Mungu, bali wa mtu aitwaye Yesu, ambaye ubinadamu wake ulikuwa nyumba ya Mungu. Hotuba za Nestori zilileta mgogoro mkubwa na upinzani ulitoka kila upande kupinga makosa yaliyokuwa katika maelezo hayo. Askofu Sirili alimpelekea Nestori barua mbili za kidugu, lakini Nestori alirudisha majibu ya kashfa tupu.

Mji wa Konstantinopoli siku zile ulikuwa na hadhi kubwa katika ulimwengu wa siasa, hasa kama makao ya Kaisari. Hii inaeleza kwamba Nestori hakuvumilia kusahihishwa na Askofu wa Aleksandria. Tena katika kutetea imani, Askofu Sirili alifuata mapokeo ya Aleksandria yanayojulikana katika historia kama 'Shule ya Aleksandria', yanayotegemea sana sala na imani. Lakini Nestori aliwakilisha 'Shule ya Antiokia', inayothamini zaidi elimu na historia.

Sehemu zote mbili walimwomba Papa Selestini ambaye aliyachunguza mambo hayo katika Mtaguso Mkuu wa Roma (Italia). Baadaye Papa alitoa tamko kwamba Nestori alipaswa kujiuzulu kama angekataa kubadili usemi wake. Askofu Sirili aliteuliwa kuitekeleza hukumu iliyotolewa, na kuhakikisha kwamba Nestori anajirekebisha. Lakini baadaye Nestori aliendelea tena na mafundisho yake ya kupotosha imani na kuwa mkaidi kuliko alivyokuwa mwanzoni.

Jambo hili lilisababisha kuitishwa kwa Mtaguso Mkuu huko Efeso (Uturuki), mwaka 431. Mtaguso huo ulihudhuriwa na Maaskofu wapatao mia mbili pamoja na Sirili, akiwa kama Askofu Mkuu na Mwakilishi wa Baba Mtakatifu. Nestori alikuwa pale mjini karibu na Efeso, lakini hakutaka kuhudhuria kikao hicho. Mafundisho yake yalitangazwa kuwa ni makosa, alitengwa na Kanisa, pia alitakiwa kujiuzulu.

Lakini Nestori hakujali. Aliita mkutano wa Maaskofu wachache waliomwunga mkono. Pia, alifaulu kujipendekeza kwa Kaisari mpaka mwishowe Sirili alipofungwa kwa amri ya Kaisari. Sirili alivumilia, hakupiga kelele, bali alisisitiza mafundisho ya Efeso. Baada ya kifungo cha miezi kadhaa, alifaulu kwa msaada wa dada yake Kaisari, Pulkeria, kurudi jimboni kwake. Kaisari Teodosi, aliyempendelea kwanza Nestori, sasa alitambua haki ya Sirili na kumfukuza Nestori katika Jimbo lake.

Baada ya kurudi Aleksandria, Sirili alijaribu kutafuta uwezekano wa kuwasahihisha wale wafuasi wa Nestori. Aliandika baadhi ya Maandishi. Alikuwa mwanateolojia kuliko Askofu, ndivyo anavyoheshimiwa mpaka hivi leo. Alikufa mwaka 444. Alitajwa kuwa Mwalimu wa Kanisa mwaka 1892.

*MT. SIRILI WA ALEKSANDRIA, UTUOMBEE*

*MASOMO YA MISA*

I. Mwa. 13:2,5-18

Zab. 15:1-5

INJILI. Mt. 7:6,12-14