Catholic Diocese Malindi

slider10.jpg
slider5.jpg
slider8.jpg
slider6.jpg
slider11.jpg
slider9.jpeg
previous arrow
next arrow

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko Dominika tarehe 9 Julai 2023 amewateuwa Makardinali wapya 21 kati yao Makardinali watatu ni wale ambao wamejipambanua katika huduma kwa Kanisa na watu wa Mungu katika ujumla wao.

Makardinali kimsingi ndio washauri wakuu wa Khalifa wa Mtakatifu Petro ili kukoleza juhudi za toba, haki, amani na maridhiano; kwa kukuza na kudumisha utu na heshima ya binadamu, ili watu waweze kuishi katika mazingira bora zaidi. Makardinali wapya watasimikwa rasmi katika mkutano wa kawaida wa Makardinali utakaoadhimishwa tarehe 30 Septemba 2023 mjini Vatican.

Hawa ni Makardinali wanaoonesha ukatoliki wa Kanisa, wanaotumwa kutangaza na kushuhudia upendo wa huruma ya Mungu kwa watu wote wa Mataifa. Makardinali hawa wataingizwa kwenye Jimbo kuu la Roma ili kuonesha mahusiano na mafungamano kati ya Khalifa w Mtakatifu Petro na Makanisa mahalia yaliyoenea sehemu mbalimbali za dunia.

Uteuzi wa Makardinali wapya ni changamoto kubwa inayowataka kujizatiti zaidi katika kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo Yesu, kwa kuhakikisha kwamba, imani inamwilishwa katika matendo; daima wakijielekeza zaidi katika huduma kwa watu wa Mungu sehemu mbalimbali za dunia.

Makardinali wanaojitambulisha kwa mavazi mekundu, wanaitwa kusadaka maisha yao kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake, tayari kuwashirikisha watu wa Mataifa, ile furaha ya Injili.

Ni mwaliko wa huduma makini kwa watu wa Mungu. Jicho la kibaba linalooneshwa na Baba Mtakatifu Francisko kwa maskini na wale wote wanaosukimizwa pembezoni mwa jamii, ni chachu ya matumaini na mapendo ambayo yanapaswa kutawala katika maisha ya watu!

Baba Mtakatifu Francisko tarehe 13 Aprili 2023 alimteuwa Askofu mkuu Protase Rugambwa kuwa Askofu mkuu mwandamizi mwenye haki ya kurithi Jimbo kuu la Tabora, Tanzania.

Makardinali ni washauri wakuu wa Khalifa wa Mtakatifu Petro
  

Askofu mkuu Robert Francis PREVOST, O.S.A., Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa; Askofu mkuu Claudio GUGEROTTI, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Makanisa ya Mashariki;

Askofu mkuu Víctor Manuel FERNÁNDEZ, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa, Askofu mkuu Emil Paul TSCHERRIG, Balozi, Askofu mkuu Christophe Louis Yves Georges PIERRE, Balozi, Askofu mkuu Pierbattista PIZZABALLA, Patriaki wa Madhehebu ya Kilatini mjini Yerusalemu: 

Askofu mkuu Stephen BRISLIN, wa Jimbo kuu la Cape Town, Afrika ya Kusini,  Askofu mkuu Ángel Sixto ROSSI, S.J., wa Jimbo kuu la Córdoba; Askofu mkuu Luis José RUEDA APARICIO, wa Jimbo kuu la Bogotá; Askofu mkuu Grzegorz RYŚ, wa Jimbo kuu la Łódź, Askofu mkuu Stephen Ameyu Martin MULLA, Jimbo kuu la Juba, Sudan ya Kusini;

Askofu mkuu José COBO CANO, wa Jimbo kuu la Madrid, Askofu mkuu mwandamizi Protase RUGAMBWA, wa Jimbo kuu la Tabora, Tanzania;  Askofu mkuu Sebastian FRANCIS, wa Jimbo kuu la Penang; Askofu Stephen CHOW SAU-YAN, S.J., Askofu wa Hong Kong:

Askofu François-Xavier BUSTILLO, O.F.M. Conv., wa Jimbo la Ajaccio, Askofu msaidizi Américo Manuel ALVES AGUIAR, wa Jimbo kuu la Lisbon, Ureno pamoja na Padre Ángel FERNÁNDEZ ARTIME, s.d.b., Mkuu wa Shirika la Wasalesian wa Don Bosco. Makardinali wapya wanasimikwa tarehe 30 Septemba 2023

Makardinali wengine katika orodha hii ni wale ambao wamejipambanua katika huduma kwa watu wa Mungu ni pamoja na Askofu mkuu Agostino MARCHETTO, Balozi; Askofu mkuu mstaafu Diego Rafael PADRÓN SÁNCHEZ, wa Jimbo Cumaná; Padre Luis Pascual DRI, OFM Cap., Muungamishi wa Madhabahu ya Mama Yetu wa Pompei, Buenos Aires nchini Argentina.

Baba Mtakatifu anawaalika watu wa Mungu kuwakumbuka na kuwaombea Makardinali hawa wapya, ili waendelee kushikamana na Kristo Yesu Kuhani Mkuu mwenye rehema, mwaminifu katika mambo ya Mungu, huku wakiendelea kumsaidia Baba Mtakatifu, Khalifa wa Mtakatifu Petro katika kutekeleza dhamana na wajibu wake kama Askofu wa Roma kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu waaminifu wa Mungu.