Catholic Diocese Malindi

slider10.jpg
slider5.jpg
slider8.jpg
slider6.jpg
slider11.jpg
slider9.jpeg
previous arrow
next arrow

Karibuni wapendwa wa Mungu kwa adhimisho la Misa Takatifu asubuhi ya leo. Katika somo la kwanza Mungu anamtokea Abrahamu akiwa karibu na mialoni ya Mamre. Hapa ni nyumbani kwa Abrahamu alipofikia baada ya kutoka Misri, hapa alijenga hapo madhabahu ya Bwana na ndipo alipozikwa yeye, Sarah na Isaka.

Katika somo letu la leo Abrahamu akiwa nyumbani, Mungu anamtokea akiwa katika wageni watatu. Abrahamu anawaona na anawachangamkia sana na kusujudu. Yeye anaenda bandani kutafuta mwana ndama na anamweleza Sara mkewe aandae mikate saafi.

Hapa Abrahamu anaenda bandani mwenyewe, wala hatumi mtu. Ishara ya unyofu na kujituma. Sara naye anaanda mikate mwenyewe. Hapa tujifunze wale tunaowatuma wafanyakazi watufanyie kila kitu. Isije ikafikia mahali ukawaambia wasali kwa niaba yako ili wewe ulale au unawalipa watu hela wakafagie kanisa kwa niaba yako. Utashindwa kukutana na Mungu katika majitoleo yako.

Abrahamu anakuwa mkarimu sana. Na Mungu anampa baraka nakumkushusha juu ya agano lake la kumpa uzao.

Tujifunze kuwa wakarimu kwa watu. Tusiwe watu wakufukuza wageni na kukwepa watu, siku unaweza ukamfukuza Mungu au ukamkwepa.

Wazee wanasema, "anaye wafukuza wageni kila mara kuna siku atawafukuza malaika". Tujitoe kwa ajili ya Mungu na wenzetu ili Mungu atubariki. Ukarimu wa Abrahamu unamfungulia laana ya miaka mingi yakutopata mtoto.

Ndugu zangu tuwe wakarimu kwa Mungu, tutoe zaka, tutoe sadaka na michango ya kanisa, itatufungulia baadhi ya baraka ambazo pengine hatukuwahi kuzipata maishani mwetu. Mungu ana nguvu ajabu, hashindwi kitu.

Katika somo la Injili Yesu anashangazwa kabisa na Imani kubwa ya Akida wa Kirumi. Kutaka mtumishi wake aponywe kwa neno la Yesu bila hata ya kuguswa kwa mkono. Hili lilimshangaza Yesu kwani linafanywa na mtu ambaye sio Myahudi, ni jemedari wa Kirumi.

Ndugu zangu, sisi tunaamini nguvu ya neno la Yesu? Au nilazima tukanyage mafuta kwa kisigino ndio tuamini kwamba tutapona? Ukosefu wa imani umewafanya wengi wakadhalilika na kutumika kama mtaji kwa waganga na manabii wa uongo. Tumuombe Yesu atusaidie tuliamini Neno lake ambalo ni uzima, lenye nguvu ya kuponya kila aina ya jeraha.

Neno hili linatufaa sana siku hizi kwani tunayasikia maneno ya Yesu zaidi kuliko kumuona kwa macho yetu ya kawaida. Amini nguvu ya neno la Mungu, linatoa uponyaji wa hali ya juu.

Kama Yesu alivyowaponya wagonjwa wengi. Nasi wakosefu tupo wengi wa kila aina. Turuhusu neno lake lituguse zaidi na kutufanya wapya.

©️ Pd. Prosper Kessy OFMCap.