slider10.jpg
slider5.jpg
slider8.jpg
slider6.jpg
slider11.jpg
slider9.jpeg
previous arrow
next arrow

TAFAKARI YA MASOMO YA DOMINIKA YA 25 YA MWAKA A WA KANISA*

*Na Padre Kelvin Onesmo Mkama, Jimbo Kuu Mwanza*

*SOMO LA KWANZA: Isa. 55:6-9*

Somo letu la kwanza linatukumbusha kuwa *“tukiacha njia zetu mbaya tutapata msamaha wa Mungu.”* Unabii huu wa Isaya ulitolewa wakati Waisraeli wakiwa uhamishoni Babeli. Waisraeli walifahamu wazi kuwa wamechukuliwa na kupelekwa uhamishoni Babeli kama adhabu kutoka kwa Mungu kwa dhambi walizotenda.  

Hata hivyo mawazo yao wakiwa Babeli yalikuwa hasi: walidhani Mungu amewatelekeza mazima mazima, walidhani Mungu hawajali tena, walifikiri Mungu amewachukia kabisa kwa sababu ya dhambi walizotenda na ya kwamba hawana nafasi tena mbele ya Mungu. Hayo yalikuwa ni mawazo yao lakini mpango wa Mungu  haukuwa kuwatelekeza bali kulitakasa taifa lake kwa njia ya mateso huko Babeli. Mungu ameruhusu wapelekwe uhamishoni siyo kwa lengo la kuwaangamiza bali kuwatakasa, yaani aliruhusu wapelekwe uhamishoni kwa lengo la kuwarudi (kama ambavyo mzazi humwadhibu mtoto wake ili kumfunza nidhamu).

Ama kweli mawazo ya Mungu siyo mawazo ya mwanadamu na njia za Mungu siyo njia zetu. Hivyo Mungu kwa kinywa cha nabii Isaya anawahakikishia Waisraeli kuwa endapo wataacha mwenendo wao mbaya atakuwa karibu nao na atawasamehe dhambi zao na kuwarudisha kwenye nchi yao ya Israeli. Haya yote yatawezekana ikiwa wataacha mwenendo wao mbaya: *“Mtu mbaya na aache njia yake.”*

Somo letu la leo linatukumbusha juu ya kuacha njia zetu mbaya ili kupata huruma ya Mungu na kurudisha ukaribu wetu na Mungu. Huruma hii ya Mungu tutaiona pia kwenye somo la Injili. Dhambi zetu hazipaswi kutufanya tujione hatufai mbele ya Mungu na kukata tamaa ya kupata msamaha wa Mungu.

Huruma ya Mungu i wazi kwa wote walio tayari kuacha njia zao mbaya (kuacha dhambi). Hatupaswi kuendelea kuenenda katika njia zetu mbaya bali kuwa tayari kuacha dhambi zetu: ubinafsi, dhuluma, majivuno, uasherati na uzinzi, rushwa, n.k. Licha ya dhambi zetu bado Mungu ana mpango na sisi. Cha msingi ni kujibidiisha kuitafuta huruma ya Mungu: kuchunguza dhamiri zetu, kujutia dhambi, kukusudia kuacha dhambi, kuungama dhambi na kufanya malipizi ya dhambi. Haya yatatuwezesha kumpata Bwana maadamu yu karibu.

*SOMO LA PILI: Flp. 1:20-24, 27*

Somo letu la pili linatoka kwenye Waraka wa Mtume Paulo kwa Wafilipi. Waraka huu Paulo aliuandika akiwa kifungoni. Kwa nini yupo kifungoni? Kitendo cha kuhubiri habari za Kristo (Injili) kwa wakati huo kilikuwa ni kosa la jinai na hivyo mitume wengi waliojihusisha na kuhubiri habari za Kristo walikamatwa, kufungwa gerezani (au kifungo cha nyumbani) na hata kuuawa.

Paulo naye amekamatwa na yupo kifungoni akisubiri hatima yake: ama kuuawa au kuachiwa huru. Naye Mtume Paulo yupo tayari kwa lolote: ikiwa atauawa kwa sababu ya kumhubiri Kristo basi itakuwa ni faida maana atakuwa ametoa maisha yake kama ushuhuda thabiti wa imani na upendo kwa Kristo na kwa kifo chake ataungana na Kristo mbinguni (hivyo kifo chake hakitakuwa hasara bali kitakuwa na faida); na ikiwa ataachiwa huru basi ataendelea kumhubiri Kristo bila uoga (ataendelea kumuungama Kristo). Kwa kuwa yupo tayari kwa lolote kati ya hayo mawili ndiyo maana Mtume Paulo anakiri kwa ujasiri: _*“Kwa maana kwangu mimi kuishi ni Kristo, na kufa ni faida.”*

Na kwa sababu yupo kifungoni (anateseka kwa ajili ya Injili), Mtume Paulo anayatazama mateso yake kama njia ya *“kumwadhimisha”* Kristo. Katika muktadha wa somo letu neno “kuadhimishwa” lina maana ya *“kutukuzwa, kuinuliwa, kukuzwa” (to be magnified, to be glorified, to be exalted).* Hivyo, Paulo anayatazama mateso ya mwili anayoyapitia (kupigwa mijeledi na kuteseka kifungoni) kama njia ya Kristo kutukuzwa, kuinuliwa, kukuzwa- yaani mwili wake (mwili wa Paulo) ni chombo cha kumtukuza Kristo kwa njia ya mateso anayopitia kwa sababu ya kuhubiri Injili. Hivyo Paulo anatufundisha jambo kubwa kuwa: *“mateso, mahangaiko, shida na taabu tunazopitia kwa njia ya mwili yana lengo la kuonesha ukuu na utukufu wa Kristo/Mungu.”

* Paulo anasema wazi kuwa “Kristo ataadhimishwa katika mwili wangu; ikiwa kwa maisha yangu, au ikiwa kwa mauti yangu.” Je, Paulo ana maana gani? Kwamba ikiwa ataachwa huru toka kifungoni na kuendelea kuishi bado mwili wake utatumika kumwadhimisha Kristo kwa huduma ya Injili na mateso yatakayomkuta, na ikiwa atauawa huko kifungoni bado kwa kifo chake atakuwa amemtukuza na kumwinua Kristo kwa kumwaga damu yake kwa ajili ya Kristo. Ndiyo maana anasema wazi kuwa anatamani kuendelea kuishi (ili azidi kumhubiri Kristo) na wakati huo huo anatamani kufa (ili kuungana na Kristo mbinguni). Ndiyo maana Paulo anasema, “Kwa maana kwangu mimi kuishi ni Kristo, na kufa ni faida”- akiendelea kuishi ataendelea kumhubiri Kristo, na hata akifa haitakuwa hasara bali faida maana ataungana na Kristo mbinguni.

Tunayo mambo kadhaa ya kujifunza kutoka kwenye somo letu la pili: *(1) Mateso/magumu tunayopitia katika hali yetu ya mwili yawe altare ya kumwadhimisha Kristo.* Mateso yetu (magonjwa, uzee, changamoto za kiimani, changamoto za ugumu wa maisha, changamoto za familia na mengineyo) yanapaswa “kumwadhimisha” Kristo: mateso na magumu yetu ni maadhimisho ya ukuu, utukufu na adhama ya Kristo/Mungu. Kila tunaposeka tufahamu wazi kuwa tunamtukuza Mungu, na kama tunamtukuza Mungu kwa mateso yetu basi naye atatutukuza huko mbinguni. *

(2) Tunapaswa kuishi kwa ajili ya Kristo.* Ikiwa Paulo ataachiwa huru toka kifungoni basi ataendelea kuishi kwa ajili ya Kristo: kumhubiri Kristo, kutimiza mapenzi ya Kristo. Wengi wetu katika maisha ya hapa duniani tu kinyume kabisa cha Paulo kwani wengi wetu tunaishi si kwa ajili ya Kristo bali kwa ajili yetu sisi wenyewe: tunajitukuza wenyewe, tunajihangaikia wenyewe, tunajitumikia wenyewe, tunafuata mapenzi yetu wenyewe. Kwa hali hii hatuwezi kamwe kutamka kwa ujasiri kama Paulo ya kwamba, “Kwa maana kwangu mimi kuishi ni Kristo.” Tukiishi kwa ajili ya Kristo tunaungana naye mbinguni, yaani tutapata tuzo la uzima wa milele pamoja naye huko mbinguni.

*SOMO LA INJILI: Mt. 20:1-16*

Katika Injili ya leo Yesu anaufananisha ufalme wa mbinguni na wakulima walioajiriwa kwa nyakati tofauti tofauti lakini mwishoni wakalipwa ujira sawa. Wakulima hawa walikuwa ni vibarua tu. Labda tuone kwanza muktadha wa somo letu.  Katika mazingira ya Kiyahudi vibarua walikuwa na maisha magumu sana. Daima maisha yao ya kila siku yalitegemea upatikanaji wa kibarua- asipopata kibarua basi angelaa njaa siku hiyo. Na kwa kawaida ujira wa kibarua ulikuwa mdogo sana, ulikuwa ni kwa ajili ya kupitisha siku- “pata ujira wako leo weka mdomoni, kesho tutajua tutaishije.”

Hivyo wengi wa vibarua walifika maeneo ya sokoni wakiwa na vifaa vya kazi kusubiri kupata kibarua. Hivyo vibarua waliofika sokoni hawakuwa wavivu- bali walifika sokoni kungojea bahati ya kupata kibarua ili kupata vijisenti vya kupitisha siku. Kwa kweli hali ya upatikanaji wa kibarua ilikuwa ngumu na ndiyo maana walisimama sokoni tangu asubuhi hadi jioni kungojea bahati ya kupata kibarua.

Licha ya ugumu wa kupata kibarua- vibarua hawakukata tamaa ndiyo maana walisimama sokoni tangu asubuhi hadi jioni. Kadhalika katika Injili ya leo inaonekana wazi kuwa  mwenye shamba alikuwa na hitaji kubwa la vibarua ili kukimbizana na muda- akichelewa kushughulikia zabibu zake mapema basi zitaharibikia shambani. Na ndiyo maana alirudi sokono mara tatu kutafuta vibarua/wakulima. 

Injili inatueleza kuwa wakulima walichukuliwa kwa nyakati tofauti tofauti tangu asubuhi hadi saa 11 jioni. Tunaona wazi kuwa mwenye shamba alifanya makubaliano na wale aliowaajiri asubuhi ya kuwalipa dinari kwa kutwa nzima; wale walioajiriwa saa 3, saa 6, saa 9 na saa 11 hakufanya nao makubalino juu ya kiasi cha kuwalipa. Mwisho wa yote ulipowadia muda wa kuwalipa wote walioajiriwa siku ile, wote walilipwa kiasi sawa. Hali hii ilizua manung’uniko kwa wale walioanza kufanya kazi tangu asubuhi maana waliwatazama wenzao kana kwamba wamependelewa maana wamefanya kazi kwa muda mfupi ukilinganisha na wao waliofanya kazi tangu asubuhi.

Hata hivyo wale walioajiriwa tangu asubuhi walisahau kuwa wamelipwa kwa kadiri ya kile walichokubaliana- Je hawajapewa dinari kama walivyokubaliana kuwa watalipwa dinari? Sasa mbona wanalalamika? Je, mwenye shamba amekiuka makubaliano? La hasha! Mwenye shamba ametimiza makubaliano yao, ametenda haki kabisa (amewalipa kiasi walichokubalina). Mfano huu wa Yesu uliwalenga Wayahudi na uliwalenga pia wanafunzi wa Yesu (disciples of Jesus). Kivipi?

Kwa somo hili Wayahudi wanakumbushwa kuwa hata kama Mungu alijifunua kwanza kwao kupitia Abrahamu na kuwafanya kuwa taifa teule, kamwe wasijione kuwa wao ni bora zaidi kuliko watu wa mataifa mengine ambao wataipokea imani baadaye. Na kwa wanafunzi wa Yesu somo hili linalenga kuwaonya kuwa licha ya wao kuwa wa kwanza kujiunga na jamii ya Wakristo lakini hawapaswi kujiona kuwa bora na wa thamani zaidi kuliko wale watakaojiunga na jamii hiyo ya Wakristo siku za mbeleni.

Kutoka kwenye Injili yetu ya leo tunafundishwa kuwa: *(1) Hata kama tumeipokea imani mapema, tujue wazi kuwa watakaoipokea imani baadaye nao ni bora mbele za Mungu kama sisi.* Vibarua walioajiriwa mapema asubuhi wanawawakilisha wale waliojiunga na jamii ya Wakristo mapema zaidi. Mara nyingi wale “waliopokea imani/ukristo mapema” hujiona wao ni bora zaidi kuliko wale waliopokea imani miaka ya karibuni. Waliopokea imani miaka za zamani hufikiri wao ndio wakristo haswa na ya kwamba wana haki ya kuamua mustakabali wa kanisa maana wana uzoefu. Hujifanya wao ndio waamuzi wa shughuli zote za Kanisa.

Utawasikia waamini wa namna hii wakisema, “utaniambia nini bwana? Mimi nimebatizwa zamani na wazungu,” Utawasikia wengine wakisema, “Sisi ndio Wakristo kweli kweli, hawa wengine ni wa juzi juzi tu.” Mfano huu unatukumbusha kuwa *“waamini wote ni sawa mbele ya Mungu”-* hakuna mkristo mwenye haki zaidi mbele za Mungu. Sisi wote ni sawa mbele ya Mungu. Kupokea imani mapema hakukupi hatimiliki ya ukristo/imani. *(2) Huruma na upendo wa Mungu havina mipaka kwani Mungu hutupatia hata kile tusichostahili.*

Katika mazingira ya kawaida na ya kutenda haki, wale walioajiriwa kwa muda mfupi tu walistahili kupata kiasi cha chini ukilinganisha na wale walioajiriwa tangu asubuhi na kufanya kazi ngumu. Hata hivyo, “mawazo ya Mungu si mawazo yenu, wala njia zetu siyo sawa na njia za Mungu” kama lisemavyo somo letu la kwanza. Utendaji wa Mungu siyo sawa na utendaji wetu. Daima huruma ya Mungu yashinda haki yake. Wakulima walioajiriwa ilihali muda umekwenda sana walipata ujira ambao kimsingi hawakustahili kupata.

Hapa tunafundishwa kuwa, *“Mungu ni mwingi wa huruma na mkarimu kwani hutupatia hata kile ambacho kimsingi hatukustahili.”* Hii ni kweli kabisa kwani pamoja na mapungufu yetu, Mungu anatupatia neema na baraka nyingi. Tunapewa yote kwa neema ya Mungu. Mungu hutupatia kwa kadiri ya upendo wake- tunachopewa na Mungu siyo malipo ya kazi nzuri tuliofanya au maisha mazuri tunayoishi bali ni neema tu. Neema ni nini? Neema ni zawadi tunayopatiwa na Mungu pasipo mastahili yetu.

Dominika njema